Ili kuweza kufahamu historia na maendeleo ya Kiswahili inatupasa kufahamu
maana ya Msawahili na Kiswahili. Mswahili ni nani? Ni swali ambalo ni la mjadala kwani baadhi ya wataalamu wamejaribu kulifafanua suala hili kwa mitazamo tafauti katika fasili zao mbali mbali kama zifuatazo;
Maganga, C. (1997), anasema Waswahili ni watu wazungumzao lugha ya kiafrika inayohusiana sana na lugha za kibantu zinazozungumzwa hivi sasa kando mwa pwani ya Kaskazini ya Kenya, Somalia na kwamba ilingiza maneno mengi ya Kiarabu katika karne chache zilizopita.
Massamba, D. (2002), akimnukuu Stigand, (1913), Waswahili ni watu waliotokana na uzao wa umoja wa Waarabu au Waajemi wa asili waliotamakani katika upwa wa Afrika ya Mashariki.
Massamba, D. (2002), Waswahili ni watu wanaoishi katika eneo la mji ambako huishi watu wa kawaida (wa hali ya chini) hii ilitokana na hali halisi ya matabaka yaliyokuwa yakijitokeza katika miji ya pwani baada ya kufika kwa wakoloni ( wa Kiarabu na Kizungu) na wafanya biashara wa Kihindi.
Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa Waswahili ni watu wa upwa wa Afrika ya Mashariki ambao lugha yao ya mawasiliano ni Kiswahili.
Kwa maana hiyo Kiswahili ni lugha inayotumiwa na watu wa upwa wa Afrika Mashariki katika shughuli zao zote za mawasiliano.
Baada ya kufahamu maana ya Kiswahili na Mswahili tunapaswa kufahamu vyanzo mbali mbali ambavyo tunaweza kutumia kupata historia ya Kiswahili kama ifuatavyo. Kuna vyanzo kama vya kihistoria, Kiakolojia, Kijiografia, Kiisimu au Kilughawiya na vyenginevyo.
Kabla ya kujadili asili ya lugha ya Kiswahili ni muhimu kufahamu maana ya neno asili.
Kwa mujibu wa Massamba na wenzake (1999), neno asili lina maana ya jinsi kitu au jambo lilivyotokea au lilivyoanza. Kuna nadharia mbali mbali zinazozungumza juu ya asili ya Lugha ya Kiswahili kama vile Kiswahili ni Kikongo, Kiswahili ni Kiarabu, Kiswahili pijini au Krioli, Kiswahili ni Kibantu na nyenginezo.
Kuhusu nadharia ya Kiswahili ni Kikongo baadhi ya wataalamu hudai kuwa asili ya Kiswahili ni huko Kongo ambayo ni Zaire ya sasa. Dai hilo linaimarishwa na wazo jengine linalodai kwamba katika vipindi kongwe vilivyopita, kuweko sehemu ya pwani ya Afrika ya Mashariki hazikuwa zimekaliwa na watu. Kutokana na vita uchungaji na biashara, inadaiwa kuwa Wabantu walitokea sehemu za Kongo na walisambaa na kuja pwani ya Afrika Mashariki kupitia Kigoma. Baadhi ya Wabantu hawa walipitia sehemu za Uganda wakati wa kusambaa kwao walieneza pia lugha zao ikiwemo hii ya Kiswahili (Msokile 1992:12).
Pia kuna madai kwamba Kiswahili ni Kiarabu. Madai hayo yanaambatana na hoja tatu kuu. Kwanza inadaiwa kuwa asilimia 41 ya maneno yote ya Kiswahili yanayoweza kuandikwa ni asili ya Kiarabu. Hoja ya pili inahusu neno lenyewe la Kiswahili ambalo asili yake ni Kiarabu. Kimsingi neno “Sahil” (Umoja) lina maana ya Pwani. Swahil (wingi) hutumika katika maana ya wingi. Na sababu ya tatu inayotolewa ni ile inayohusu shughuli mbali mbali zilizohusishwa sana na waarabu kama vile dini, biashara, utawala, mila na desturi.
Kadhalika kuna dai linasema kuwa Kiswahili ni Krioli au Pijini. Nadharia ya pijini au Krioli hutumia kigezo cha msamiati wa Kiswahili kuonesha uhusiano uliopo kati ya Kiswahili na Kiarabu. Inadaiwa kuwa msamiati mwingi wa Kiswahili unatoka na Kiarabu hivyo huhitimisha kuwa hapana shaka Kiarabu kimehusika katika kuzaliwa lugha ya Kiswahili. Udhaifu wa nadharia hii ni kuwa haitumii vigezo vya lugha kama vile matamshi, miundo ya maneno na muundo wa sentensi za Kiswahili (Masebo na mwenzake 2010).
Mbali na nadharia hizo kuna nadharia ya Kiswahili ni Kibantu. Mtazamo huu unaamini kuwa Kiswahili ni lugha ya Kibantu na lugha za Kibantu zilikuwepo hata kabla ya kuja kwa wageni kutoka Ujerumani, Uarabuni, India, China na kwengineko. Katika mtazamo huu lugha ya Kiswahili inaingizwa katika kundi la lugha za Kibantu. Vigezo vilivyotumika kufafanua kuwa Kiswahili ni Kibantu ni pamoja na;- Msamiati, Mofolojia, Mfumo wa Sauti, Mfumo wa ngeli na mpangilio wa maneno. Hata hivyo kila hoja ina maelezo ya kina katika kujadili kile wanachokiamini. Makundi mengi ya wataalamu wanaelekea kukubaliana na dai la kuwa Kiswahili kimetokana na Kibantu kutokana na hoja mbali mbali zilizoainishwa.
Kwa upande wa chimbuko la lugha ya Kiswahili limejadiliwa na wataalamu wengi. Mijadala yao imeambatana na kauli mbali mbali zinazohusu nadharia ya chimbuko la Kiswahili. Inasemekana kuwa chimbuko la lugha ya Kiswahili ni kando kando ya upwa wa Afrika Mashariki ambapo kuna miji mingi ya awali ambayo baadhi ya wataalamu hao wanaamini kuwa ndio chimbuko la Kiswahili. Mifano miji hiyo ni kama vile eneo la Mogadishu ambapo eneo hili linapatikana Kaskazini mwa mwambao wa Afrika ya Mashari na wakaazi wake walikuwa wakitumia Kiswahili. Eneo jengine ni eneo la Manda, na linapatikana katika visiwa vya Pate ambavyo vipo katika nchi ya Kenya, eneo hili limethibitika kuwa linazungumza Kiswahili baada ya wasafiri mbali mbali kutembelea eneo hilo. Vile vile katika mji wa Kilwa nako kuna ushahidi wa miji ya kwanza kuzungumza Kiswahili. Miji mengine ni kama vile Lamu, Mombasa, Dar-es-salaam, Bagamoyo, Tanga, na Zanzibar. Vile vile katika mji wa Kilwa nako kuna ushahidi wa miji ya kwanza kuzungumza Kiswahili. Miji mengine ni kama vile Lamu, Mombasa, Dar-es-salaam, Bagamoyo, Tanga, na Zanzibar.
Tukiendele na historia ya Kiswahili kabla ya uhuru wageni walikitumia Kiswahili katika nyanja za elimu. Elimu ilitoa mchango mkubwa katika kipindi cha ujio wa wageni. Mfano katika kipindi cha Wajerumani waliiteua lugha ya Kiswahili kuwa itumike kama lugha ya kufundishia na pia kusomwa kama somo la kawaida katika shule za msingi. Baadhi ya shule hizo ni kama vile Tabora, Mpwapwa na kadhalika. Hivyo walimu na wanafunzi walijifunza lugha ya Kiswahili katika shughuli za elimu sambamba na kuifanya lugha hiyo kukuwa na kuenea katika maeneo tafauti. Waarabu nao walikitumia Kiswahili ili kufundishia watoto uislamu. Hivyo misamiati mingi ilipatikana kupitia elimu. Mfano neno Madrasa, daftari, kalamu na kadhalika ambayo hadi leo yanatumika katika lugha ya Kiswahili. Vile vile Kiswahili kilitumika katika nyanja za biashara.
Wageni walipofika katika pwani ya Afrika Mashariki waliwakuta wenyeji wakizungumza lugha ya Kiswahili. Hivyo walilazimika kutumia lugha ya Kiswahili ili kukidhi mahitaji ya mawasiliano katika biashara zao. Katika kuhakikisha biashara inakuwa vizuri Waarabu walianzisha vituo vya biashara kama vile Ujiji, Tabora n.k sambamba na kuenea kwa lugha ya Kiswahili katika sehemu tafauti na kupata mawanda mapana ya kimatumizi na watumiaji wengi.
Pia wageni walisanifisha lugha ya Kiswahili. Baada ya ujio wa Waengereza juhudi mbali mbali zilifanywa katika kueneza Kiswahili mwanzoni mwa miaka ya 1930 na vita vikuu vya pili vya dunia, Waengereza walifanya juhudi za kukisanifisha Kiswahili na kukuza istilahi zake. Mfano maneno kama “Skuli”, “Shati” n.k yote hayo yanatoka katika lugha ya kingereza. Hivyo Kiswahili kilitumika katika shughuli rasmi sambamba na kuenea sehemu tafauti za dunia.
Hata hivyo walikitumia Kiswahili katika shughuli za kilimo. Miongoni mwa mambo yaliyopelekea maendeleo ya Kiswahili katika kipindi cha ujio wa wageni ni kilimo. Mfano Wajerumani walianzisha mashamba makubwa ya mazao ya biashara kama vile katani huko Tanga na kahawa huko Kilimanjaro na Bukoba. Hivyo waliajiri idadi kubwa ya vibarua kutoka sehemu mbali mbali za nchi na lugha iliokuwa ikitumika ni Kiswahili. Hivyo Kiswahili kilikuwa na ongezeko la watumiaji na kufanya lugha hiyo kuenea katika maeneo tafauti.
Kadhali katika kipindi hicho dini zote mbili Ukiristo na Uislamu ni miongoni mwa sababu zilizosaidia kwa kiasi kikubwa kukuza na kueneza Kiswahili nchini. Kabla ya uhuru hadi sasa. Dini zote mbili huendesha mahubiri yake kwa lugha ya Kiswahili hivyo huchangia sana katika kueneza Kiswahili.
Pia vyombo vya habari vilijishughulisha sana katika kueneza na kukuza lugha ya Kiswahili. Vyombo hivyo ni kama magazeti na radio. Miongoni mwa magazeti yaliyojishughulisha sana na uandikaji wa Makala mbali mbali yanayohusu lugha ya Kiswahili ni kama Msimulizi (1888), Habari za mwezi (1894), Pwani na Bara (1910) Rafiki yangu (1890), Habari leo (1954), Kiongozi (1950) Mwangaza ( 1923), Sauti ya pwani (1940) na Mazungumzo ya Walimu wa Unguja (1954) n.k. Baadhi ya magazeti hayo kulikuwa na ukurasa maalumu unaohusu taaluma ya lugha ya Kiswahili. Gazeti Mambo leo liliandika mashairi na hadithi mbali mbali za fasihi simulizi. Kwa upande wa redio Tanganyika ilianzisha matangazo yake kwa kutumia lugha ya Kiswahili mnamo miaka ya 1950. Wakati wote redio iliendelea kutangaza matangazo yake kwa Kiswahili. Hii kwa kiasi kikubwa ilichangia kukuza na kueneza Kiswahili Tanzania.
Maendele ya lugha ya Kiswahili yalichukuwa sura mpya mara tu baada ya uhuru. Harakati zilizochukuliwa na serikali ya Tanzania zilipelekea maenedeleo makubwa ya lugha ya Kiswahili. Mnamo mwaka 1964 lugha ya Kiswahili iliteuliwa kuwa lugha ya Taifa. Lugha hii ilitumika katika shughuli zote za kitaifa. Massamba na wenzake (2004) “ mikutano yote iliyohusiana na wananchi mijini na vijijini iliendeshwa kwa lugha hii ya taifa”. Hivyo Kiswahili kilihimizwa kutumika katika mawasiliano yote hususani katika shughuli za umma na Wizara zote pamoja na Bunge.
Jambo jengine lililopelekea maendeleo ya lugha ya Kiswahili baada ya uhuru ni kuudwa kwa vyombo mbali mbali vya kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili. Vyombo hivyo vilikuwa na majukumu makubwa kama vile kuendeleza usanifishaji lugha, kuunda istilahi na kutaarisha viiarida na vitabu ambavyo viliweza kusaidia waswahili na wale ambao wanifunza lugha ya Kiswahili. Mfano wa vyombo hivyo ni BAKITA, TAKILUKI, BAKIZA, BAMITA, UWAKIVITA na kadhalika. Vyombo hivi vilisaidia sana maendeleo ya Kiswahili kutokana na kazi zao kwa kila chombo (Massamba na wenzake 2010) Kuanzishwa kwa vyombo mbali mbali vya habari viliendelea kutumia Kiswahili kwa kiasi kikubwa vyombo hivyo ni magazeti, majarida, radio, na runinga. Ambavyo vilitangaza kwa lugha ya Kiswahili. Mifano ya redio hizo ni kama radio Nuru, Adhana, Radio one, Redio Free Afrika n.k. Mifano ya runinga ni ITV, Star TV. ZBC, TBC na nyenginezo.
Pia Kiswahili kinaendele kutumika katika shughuli za elimu katika shule za msingi kama ni lugha ya kufundishia na sekondari na vyuo vikuu ambavyo wanatoa shahada mbali mbali pamoja na uzamini na uzamivu wa somola kiswahili. Kiswahili kiliendelea kutawanya mawanda yake barani Afrika na duniani kwa ujumla.
Elimu ya watu wazima ambayo huwajumuisha watu wazima kusoma na kuandika.Watu hawa hujifunza kiswahili nakupelekea kuweza kusoma nakuandika na kuzungumza kwa lugha ya kiswahili fasaha. Masamba (2010) anasema “nchini kote elimu ya watu wazima imefundishwa kwa kiswahili kupitia masomo tofauti kama vile ufundi, siasa, kilimo, na afya. Hali hii ilisaidia maendeleo makubwa ya Kiswahili hapa nchini. Licha ya hayo maendeleo ya Kiswahili yanakuwa na kuenea sehemu mbali mbali kwa kupitia shughuli za biashara, shughuli za kisiasa, uchapishaji wa vitabu vya sarufi na fasihi, shughuli za utamaduni pamoja na harakati mbali mbali.
Ukuaji na ueneaji wa Kiswahili duniani Msokile, M (1992) anadai kuwa lugha ya Kiswahili hivi sasa imepenya sehemu nyingi duniani. Kiswahili kinazungumzwa Afrika Mashariki nzima, Somalia, Msumbiji, Afrika ya Kusini, Zimbabwe, Angola, Zaire, Zambia, Ruwanda, Burundi, Nigeria, Sudan na Misri. Nje ya Afrika kuna vyuo vikuu, vituo vya redio na televisheni vinavyoshughulikia lugha ya Kiswahili. Mfano wa vituo vya redio ni Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran katika nchi ya Iran, Redio ya China Swahili, BBC Swahili London. Inasemekana hivi sasa kuwa kuna watu zaidi ya milioni 1000 wanzungumza Kiswahili duniani. Ushahidi wa hayo tunaona kuwa Papa John wa pili alitembelea Tanzania mnamo tarehe 1/06/1990 alitumia lugha ya Kiswahili. Pia Kiswahili sasa kinaendelea kutumika katika kutafsiri nyaraka mbali mbali, mitandao au tovuti, sharia, biashara, na uhakiki wa maandishi kuanzia wakati huo hadi sasa.
Pamoja na umaarufu wa lugha ya Kiswahili dunia, lakini bado lugha hii inaendelea kukukabiliana na changamoto nyingi. Kwa mujibu wa Dafina ya Kiswahili (2014) wamebainisha changamoto kama zifuatavyo;
Katika dhana ya Kiswahili bado kuna baadhi ya watu wanaonasibisha kiswahili na dini ya kiislam hili limekuwa ni tatizo kubwa miongoni mwa watumiaji wa lugha hii.
Pia upinzani mkubwa kutoka katika lugha ambazo zimekwisha jitanua katika dunia, mfano Kiingereza, Kifaransa, Kireno na Kiarabu. Watumiaji au watu wenye asili na lugha hizo wanakipiga vita kiswahili wakihofia kuwa wasipofanya hivyo kitazimeza lugha zao.
Kudharauliwa kwa lugha ya Kiswahili na kupigiwa chapuo kwa lugha za kigeni kwamba ndio pekee zinazofaa kutumika katika shughuli mbalimbali za kiuchumi. Hivyo Kiswahili kuonekana kuwa hakifai kutumiwa katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Kasumba mbaya na mtazamo hasi katika lugha ya Kiswahili ambao unawafanya watu kukitukuza zaidi Kiingereza na kutojua kuwa kiingereza ni sawa na lugha nyingine tu.
Kucheleweshwa kwa maamuzi ya sera ya kukipa hadhi kiswahili kuwa lugha ya kufundishia katika nyanja zote za elimu, na kiingereza kuwa somo tu. Hivyo inarudisha nyuma maendeleo ya Kiswahili.
Wasomi wengi kuwa nyuma katika kufanya tafiti mbalimbali juu ya lugha ya Kiswahili ili kuona ni jinsi gani tunaweza kufunguka kiakili na kufahamu umuhimu wa kuwa na lugha ya Kiswahili.
Uchumi mdogo nao unakwamisha kwa sehemu kubwa maendeleo ya haraka ya lugha ya Kiswahili duniani. Kwa kuwa nchi nyingi zinashindwa kuzalisha wataalamu wengi wa lugha hii, pia zinashindwa kufasiri maandiko kutoka lugha nyingine kuwa katika lugha ya Kiswahili kwa sababu ni ghari mno.
Wazawa wa lugha hii wanakosa moyo wa kuthamini na kujali tamaduni zao ambapo Kiswahili ni lugha inayotangaza utamaduni wao lakini wao wanathamini sana utamaduni wa kimagharibi. Kwa hakika hii ni changamoto kubwa ambayo inakikumba Kiswahili katika harakati zake za kujitanua duniani kote.
Pia kuna dhana kuwa Kiswahili ni lugha ya watu duni kitaaluma mathalani watu walioishia darasa la saba. Hivyo hufanya watu kutaka kujifunza Kiingereza. Hii ni dhana ya watu potofu kabisa ambayo inajitokeza kwa watu ambao ni wasomi kabisa.
Kwa upande wa matumizi ya lugha ya Kiswahili, kumekuwa na matatizo makubwa ya kutumiwa isivyosahihi na matumizi yasiyofasaha katika nyanja zake za kimatamshi, kimaandishi na kimaana. Matatizo hayo ndiyo yanayopelekea kutokuwa na Kiswahili sahihi na fasaha. Jambo la kusikitisha na kushtua zaidi ni kuwa kwa muda mrefu, kumebaini na kuwa na Kiswahili sanifu lakini Kiswahili hiki kinazungumzwa na kuandikwa kimakosa mno. Makosa haya hutendwa na taasisi mbalimbali zikiongozwa na vyombo vya mawasiliano. Mfano katika magazeti waandishi wanatumia lugha inayokiuka misingi na kanuni za Kiswahili sanifu tunachokielewa au wanachofundishwa wanafunzi.
James, J. na Faustino, M. (2011). Wameelezea changamoto zinazoikabili lugha ya Kiswahili ni kama; ukosefu wa utashi wa kisiasa, uhaba wa wataalamu, kuwepo kwa Viswahili vingi, kasumba za kikoloni, kupenda lugha za asili, uhaba wa fedha.
Kwa ujumla, historia ya lugha ya Kiswahili ni dhana tete ambayo kila mtaalam huwa na mtazamo wake. Ni vyema kwa wasomi na wadau wa Kiswahili kufanya utafiti wa kina juu ya historia ya lugha ya Kiswahili ili kuondosha utata huo na kubaini ukweli wa historia yake. Pamoja na maendeleo ya lugha ya Kiswahili duniani bado Kiswahili kinakabiliwa na changamoto mbali mbali. Ni jukumu la wapenzi wa lugha hii kuziangalia kwa kina changamoto hizo ili kuimarisha maendeleo yake.
MAREJEO
Maganga, C (1997) Historia ya Kiswahili. Dar-es-salaam. Chuo kikuu huria.
Massamba na wenzake (1999) Sarufi Miundo Kiswahili Sanifu Sekondari na Vyuo: Dar-es-salaam TUKI.
Massamba, D. (2002). Historia ya Kiswahili. Nairobi: The Jomo Kenyata Foundation.
Masebo, J. A (2002) Kiswahili Kidato cha 3 na 4. Dar-es –salaam Nyambari Nyangwine Publisher.
Msokile, M (1992) Historian a Matumizi ya Kiswahili. Dar-es-salaam: Chuo Kikuu cha Dar-es-salaam.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments: