Juhudi za kuikuza lugha ya Kiswahili nchini Tanzania , Barani Afrika na duniani kote zimeanza kuzaa matunda kwa kuendelea kutumiwa na watu wengi zaidi ambao ndiyo msingi wa lugha yenyewe.
Kuzinduliwa kwa Kamusi Kuu ya Kiswahili hivi karibuni Bungeni mjini Dodoma imekuwa ni chachu katika kukuza na kusimamia matumizi sahihi na fasaha ya lugha hii miongoni mwa watumiaji wake.
Uzinduzi wa kamusi hiyo ni ishara njema ya kukijenga na kukiimarisha Kiswahili ili kiweze kutumika kwa ufasaha katika nyanja zote za maisha ikiwemo elimu katika ngazi zote ,kijamii, kisiasa na kiuchumi ndani na nje ya nchi.
Akizindua Kamusi hiyo mjini Dodoma, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amewasisitiza Watanzania kujivunia kilicho chao kwa kuitumia lugha hii katika shughuli zote rasmi za kitaifa ikiwemo mikutano, mijadala, semina na ufundishaji shuleni.
Hakika lugha ya Kiswahili imeendelea kuwa ngao na nguzo muhimu kwa ustawi wa taifa na katika kulinda umoja wa kitaifa kwa Watanzania kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.
Kutokana na umuhimu wake, Waziri Mkuu anasema “Serikali inatambua umuhimu wa lugha ya Kiswahili kwa ustawi wa nchi yetu na katika kulinda umoja wa kitaifa. Hakika lugha ya Kiswahili ndiyo inayotufanya tuwe Watanzania. Hivyo, tuithamini kwani ni lulu na tunu ya Taifa”
Zaidi ya hayo Waziri Mkuu Majaliwa amempongeza Rais John Pombe Magufuli kwa kutumia lugha ya Kiswahili na kutoa mfano ambapo Rais aliyumia lugha hiyo kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika mwaka 2017, “Mheshimiwa Rais alitumia Kiswahili kuhutubia mkutano huo na amekuwa akifanya hivyo, hata kwenye mikutano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Lengo lake ni kuitangaza lugha hii” alisema Waziri Mkuu Majaliwa..
Watanzania tuna kila sababu ya kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, kwa raghba, uzalendo, jitihada, uungwana kwa kujivunia kutumia lugha ya Kiswahili kama utambulisho wa Taifa na Utamaduni wa Mtanzania.
Hatua hiyo ya Rais Dkt. Magufuli imeshadidisha matumizi ya lugha ya Kiswahili kuwa iwe mwanzo mpya kwa viongozi na jamii kwa ujumla kuipenda na kuitumia mara zote wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku ya kitaifa na kimataifa.
Mafanikio ya kuandika na kuchapisha Kamusi Kuu ya Kiswahili si ya kubeza, Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) limeendelea kuwa kisima cha hazina ya lugha hii, na wanapaswa kupongezwa na kutiwa moyo kwa kazi hii nzuri na kuwa mstari wa mbele katika kusimamia.
Awali Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe aliwaaambia Wabunge, wageni waalikwa na Watanzania wote kuwa Kiswahili ni lugha ya pili inayotumiwa na watu wengi zaidi barani Afrika na pia ni lugha ya 10 kati ya 6,000 zinazozungumzwa na watu wengi duniani.
Hakika hatua ya kutumia kugha ya Kiswahili barani Afrika na duniani ni ya kupongezwa na wadau wote wa lugha kwa juhudi za makusudi wanazozichukua za kuifikisha lugha hii kwa watumiaji wengi zaidi na kuwa kiunganishi cha mataifa mengi.
Kamusi hiyo umeshadidisha na kubidhaisha lugha ya Kiswahili na kukipa thamani ya kuweza kurahisisha mawasiliano na kuongeza idadi ya watumiaji wa lugha hiyo.
Aidha, katika Hotuba yake Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa mwaka 2017/2018 aliyowasilisha Bungeni, Waziri Dkt. Mwakyembe alisema kuwa BAKITA imepewa jukumu la kulinda na kukuza lugha ya Kiswahili ambapo pamoja na mambo mengine Kamusi ndiyo mzizi wa lugha na wamefanikiwa kuratibu na kutoa huduma za tafsiri na ukalimani kwa Asasi na Mashirika mbalimbali, watu binafsi pamoja na mikutano ya Kimataifa.
Hatua ya ukusanyaji wa Istilahi 300 za magonjwa ya mimea kwa ajili ya Kamusi ya magonjwa ya mimea; kuhariri kamusi ndogo za lugha tatu ambazo ni Kiswahili-Kiingereza-Kifaransa, Kiswahili-Kiingereza-Kireno na Kiswahili-Kiingereza-Kiarabu imedhihirisha umahiri wa BAKITA katika usimamizi na ulezi wa lugha hii.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai, katika hotuba yake iliyosomwa na Mwenyekiti wa Bunge hilo Azzan Mussa Zungu wakati wa uzinduzi wa Kamusi hiyo amesema Bunge linaendelea kusimamia matumizi ya Kiswahili katika shughuli zake za kila siku na kusisitiza Bunge litakuwa kituo cha maendeleo ya Kiswahili.
Naye Balozi wa Kiswahili Afrika na Mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Afrika Mama Salma Kikwete amesema kuwa Kamusi Kuu ya Kiswahili ni fahari ya Watanzania, itasaidia watu kujua na kutumia lugha hiyo kwa ufasaha kwenye maeneo stahiki kwa maendeleo ya Watanzania, Waafrika na duniniani kote.
“Kiswahili kikitumika ndani ya Bara letu la Afrika, kila mtu atajivunia kuwa na lugha hii, ni fahari yetu sisi kama Waafrika kuwa na lugha yetu ambayo ni Kiswahili. Kwani kila mwanandamu ana kitu chake cha asili, sisi kama Waafrika tuna lugha yetu ya Kiswahili” alisema Balozi huyo wa Kiswahili Afrika.
Akitoa taarifa kabla ya kuzinduliwa Kamusi hiyo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Dkt. Seleman Sewangi alisema kuwa Kamusi hiyo imeundwa kwa lugha ya Kiswahili na ina jumla ya maneno 45,500 ambapo kazi ya kuiandaa kamusi hiyo ilianza Agosti 12, 2011. Kamusi hiyo ilikamilika na kuchapishwa toleo la kwanza mwaka 2015.
Ni wajibu wa kila mtu wakiwemo, Viongozi wa Serikali, mashirika ya yasiyo ya kiserikali, wakuu wa taasisi za elimu na wazazi, mmoja mmoja kuhakikisha kuwa wanapata kamusi hiyo ambayo ni moja ya nyenzo za kukuza na kujifunza lugha sanifu ya Kiswahili.
Katika kutekeleza majukumu ya kila siku, Waheshimiwa wabunge, wanahabari, wakalimani, wafasiri, waandishi na wahariri wa vitabu, maofisa mawasiliano ni vema kuwa na Kamusi hiyo ili iwasaidie kujiimarisha kwenye matumizi ya Kiswahili.
Balozi wa Kiswahili Afrika Mama Salma Kikwete amewaasa Watanzania kutumia Kamusi hiyo ili kujiongezea elimu kuhusu lugha hii.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
No comments: